30 Agosti 2019 - 19:18
 Zarif: Lazima Marekani isitishe ugaidi wa kiuchumi na irejee JCPOA, kabla ya mazungumzo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amesema Marekani lazime irejee katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na isitishe ugaidi wake wa kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kabla ya kufanyika mazungumzo.

ABNA: Akizungumza Alhamisi kabla ya kuondoka Kuala Lumpur nchini Malaysia,  Zarif alisema: "Marekani inatekeleza vita vya kiuchumi dhidi ya watu wa Iran kwa hivyo haiwezekani sisi kufanya mazungumzo na Marekani hadi pale itakapositisha vita na ugaidi wa kiuchumi dhidi ya watu wa Iran." Amesisitiza kuwa, sharti la Iran kufanya mazungumzo na Marekani ni nchi hiyo isitishe ugaidi huo wa kiuchumi na irejee katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA.

Zarif pia amesema Iran haitaki kufanya mazungumzo yasiyo na maana kwa ajili tu ya kukutana  bali inataka mazungumzo ambayo yatakuwa na manufaa.

Zarif ametoa kauli hiyo siku kadhaa baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kubainisha matumaini kuwa Rais Hassan Rouhani wa Iran atakutana na Rais Donald Trump wa Marekani katika 'kipindi cha wiki chache zijazo.'

Rais Rouhani ametupilia mbali uwezekano wa mazungumzo kama hayo huku akisisitiza kuwa, Marekani kwanza isitishe vikwazo vya kidhalimu na ianze kuheshimu haki za Iran kama hatua ya kwanza ya kuelekea katika mazungumzo.

Baada ya hatua ya upande mmoja na ya kuhalifu sheria iliyochukuliwa na Marekani mnamo mwezi Mei 2018 ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ilitekeleza kwa muda wa mwaka mzima kile ilichokiita "subira ya kistratejia" na kutoa muhula kwa pande zingine hususan nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao za kufidia kujitoa Marekani kwenye makubaliano hayo.

Kutokana na kushindwa kufanya hivyo, kuanzia Mei 8 mwaka huu, Iran ilianza kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA kulingana na vifungu vya 26 na 36 vya makubaliano hayo.

Baada ya awamu mbili za utekelezaji wa hatua hizo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonya kuwa itatekeleza awamu ya tatu na kali zaidi ya kupunguza uwajibikaji huo, endapo upande wa Ulaya hautatekeleza ahadi na majukumu yake kulingana na muhula mwengine uliopewa.

...............

300